Maumivu ya mfupa wa mkia wa mgongo, ambayo pia hujulikana kama Coccygodynia, coccalgia, coccygeal neuralgia, ni tatizo linaloambatana na dalili za maumivu yanayotokea katika eneo la mfupa wa mkia (coccyx).
Maumivu haya hujitokeza mara nyingi wakati mtu ameketi, lakini pia yanaweza kujitokeza mtu anapobadilika kutoka kuketi hadi kusimama. Mara nyingi maumivu haya hupotea ndani ya wiki chache hadi miezi kadhaa, lakini kwa baadhi ya wagonjwa, maumivu yanaweza kuwa sugu na kuathiri ubora wa maisha.
Tafiti zinaeleza kwamba tatizo hili lipo mara tano zaidi kwa wanawake kuliko wanaume, labda kwa sababu mfupa huu unaonekana zaidi kwa wanawake. Ingawa coccygodynia inaweza kutokea kwa watu wa rika mbalimbali, umri wa wastani wa kuanza kwa hali hii ni takriban miaka 40.
Katika makala hii nitaeleza sababu, dalili na tiba ya tatizo hili la maumivu ya mfupa wa mkia wa mgongo.
Sababu Zinazoweza Kusababisha Maumivu ya Mfupa wa Mkia wa Uti wa Mgongo
1. Jeraha au Kuumia
Hii ni mojawapo ya sababu kuu za maumivu ya mfupa wa mkia. Inaweza kutokea mtu akiangukia kwa nguvu kwenye makalio au ajali zinazohusisha mgongo wa chini.
Kwa wanawake, kujifungua pia huweza kusababisha mfupa wa mkia kusukumwa au kuvunjika wakati mtoto anapopita kwenye njia ya uzazi. Maumivu yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya muda mrefu kulingana na ukubwa wa jeraha.
2. Kukaa kwa Muda Mrefu
Kukaa kwa muda mrefu hasa kwenye viti vigumu, vyembamba au visivyo na mto, huweka uzito mwingi kwenye eneo la mkia wa uti wa mgongo. Hii husababisha maumivu ya kukandamizwa ambayo yanaweza kuongezeka kwa muda bila mabadiliko ya mkao au mapumziko ya mara kwa mara.
3. Mabadiliko ya Mifupa kwa Sababu ya Uzee
Kadri mtu anavyozeeka, maungio ya mifupa yanapitia mabadiliko ikiwemo kulika kwa maungio.
Maungio ya mkia wa uti wa mgongo yanaweza kuwa magumu na kupoteza unyumbufu wake wa kawaida, au kuanza kusogea kupita kiasi, hali inayoweza kuleta maumivu ya mara kwa mara hasa wakati wa kukaa au kusimama ghafla.
4. Mijongeo ya Kurudiarudia
Shughuli kama kuendesha baiskeli, kupanda farasi, au kuendesha mashua huhusisha harakati za kurudia rudia ambazo huweka msongo kwenye mfupa wa mkia.
Msuguano huu wa kila mara unaweza kusababisha kuvimba au maumivu yanayoendelea, hasa kama hakuna mapumziko ya kutosha kati ya mazoezi.
5. Mkao Mbaya
Kukaa kwa mkao usio sahihi – kama vile kuinama mbele kupita kiasi au kukaa bila mgongo kuungwa mkono vizuri – husababisha mgandamizo wa moja kwa moja kwenye mkia wa uti wa mgongo.
Kwa muda, shinikizo hili huathiri mishipa na misuli inayozunguka eneo hilo na kusababisha maumivu.
6. Uvimbe au Maambukizi
Ingawa ni mara chache sana, uvimbe kwenye eneo la sacrococcygeal (mfupa wa sakramu hadi mkia wa uti wa mgongo) au maambukizi kama jipu yanaweza kusababisha maumivu makali.
Hali hizi huhitaji uchunguzi wa kitabibu haraka kwa sababu mara nyingine zinaweza kuhusisha saratani au bakteria hatari.
Maumivu ya Mfupa wa Mkia wa Uti wa Mgongo Yana Dalili Zipi?
Dalili za maumivu ya mkia wa uti wa mgongo zinaweza kujumuisha:
- Maumivu ya chini na yanayochoma sehemu ya mkia wa mgongo.
- Maumivu yanayoongezeka unapojaribu kutoka kwenye hali ya kuketi hadi kusimama.
- Maumivu wakati wa kwenda chooni (haswa kupitisha haja kubwa).
- Maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Dalili nyingine zinazoweza kuambatana na maumivu haya ni:
- Maumivu ya mgongo
- Sciatica (maumivu yanayosambaa mguuni)
- Matatizo ya usingizi.
- Unyong’onyevu wa akili (depression).
- Wasiwasi (anxiety).
Muhimu: Maumivu ya mkia wa uti wa mgongo bila kuumia yanaweza kusababishwa kwa nadra sana na saratani inayojitokeza karibu na sehemu ya mkia au inayosambaa hadi kwenye mifupa.
Hali hii si ya kawaida, lakini ni muhimu kuifahamu. Aina mbili za saratani zinazoweza kuhusishwa na hali hii ni saratani ya tezi dume na saratani ya utumbo mpana.
Dalili za kuashiria uwezekano huu ni pamoja na ganzi au miwasho mikononi, miguuni, au maeneo ya siri, pamoja na ugumu wa kukojoa au kujisaidia. Pia, mtu anaweza kuona uvimbe unaojitokeza karibu na mkia wa uti wa mgongo.
Ikiwa dalili hizi zinajitokeza, ni muhimu kutafuta ushauri wa daktari mara moja kwa uchunguzi wa kina.
…
Sasa unaweza ukawa unajiuliza tiba ya maumivu haya ni ipi? Kwa majibu ya swali hili, tukutane kwenye makala yangu ijayo. Asante!

Physiotherapist Officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
