Utindio wa ubongo (Cerebral Palsy – CP) ni kundi la matatizo yanayoathiri uwezo wa mtu kutembea na kudumisha usawa na mkao sahihi.
Tatizo hili husababishwa na maendeleo yasiyo ya kawaida ya ubongo au uharibifu katika ubongo unaokua, ambao huathiri uwezo wa mtu kudhibiti misuli yake.
Ni hali maarufu zaidi ya ulemavu wa mwendo (movement disability) kwa watoto.
Hali hii hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine ambapo mtu mwenye utindio wa ubongo kwa kiasi kikubwa (severe cerebral palsy) anaweza kuhitaji vifaa maalum ili kutembea, au asiweze kutembea kabisa na aweze kuhitaji msaada wa maisha kwa muda wote.
Na mtu mwenye utindio wa ubongo kwa kiasi kidogo (mild cerebral palsy) anaweza kutembea kwa taabu kidogo lakini asiweze kuhitaji msaada wowote.
Watu/watoto wote wenye utindio wa ubongo hupata matatizo ya mwendo na mkao. Wengi pia huwa na hali nyingine zinazoambatana na utindio wa ubongo kama vile ulemavu wa akili, kifafa (degedege), matatizo ya kuona, kusikia au kuzungumza, mabadiliko katika uti wa mgongo (kama vile scoliosis – mgongo wa “S”) na matatizo ya viungo (kama vile contractures – kukakamaa kwa misuli au viungo).
Aina za Utindio wa Ubongo
Utindio wa ubongo umegawanyika kulingana na aina kuu ya matatizo ya mwendo (movement disorders) yanayohusika na kwa kutegemea ni sehemu gani za ubongo zimeathiriwa; pia mtu anaweza kuwa na moja au zaidi ya matatizo yafuatayo ya harakati/mwendo:
- Misuli kuwa migumu (spasticity)
- Harakati/myendo isiyoweza kudhibitiwa (uncontrolled movement – dyskinesia)
- Tatizo la usawazishaji na uratibu wa mwili (balance and coordination disorder – ataxia)
Zifuatazo ni aina kuu nne (4) za Utindio wa Ubongo:
1. Utindio wa ubongo wa aina ya Spastic
Hii ndiyo aina inayopatikana sana, ikiwakumba takribani 80% ya watu walio na utindi wa ubongo. Watu hawa huwa na msukumo mkubwa wa misuli, hivyo misuli yao huwa migumu na huathiri namna wanavyotembea au kufanya harakati. Utindio wa ubongo wa spastic huelezwa kwa kuangalia ni sehemu zipi za mwili zimeathiriwa:
- Utindio wa ubongo unaoathiri miguu (Spastic diplegia/diparesis): Ugumu wa misuli hutokea hasa kwenye miguu. Mikono huathirika kidogo au kabisa haiathiriki. Misuli ya nyonga na miguu huwa migumu na kusababisha miguu kujikunyata, kukutana katikati na kukatiza magoti (inayojulikana kama scissoring), jambo linalosababisha ugumu wa kutembea.
- Utindio wa ubongo unaoathiri upande mmoja wa mwili (Spastic hemiplegia/hemiparesis): Huathiri upande mmoja tu wa mwili, kwa kawaida mkono huathirika zaidi kuliko mguu.
- Utindio wa ubongo unaoathiri mwili mzima (Spastic quadriplegia/quadriparesis): Hii ndiyo aina kali zaidi ya utindio wa ubongo wa aina ya Spastic. Huathiri viungo vyote vinne, kiwiliwili na uso. Watu wenye hali hii huwezi kutembea na mara nyingi huwa na matatizo mengine ya maendeleo kama vile ulemavu wa kiakili, degedege pamoja na tatizo la kuona, kusikia au kuzungumza
2. Utindio wa Ubongo wa Aina ya Dyskinetic
Watu wenye utindio wa ubongo aina hii hupata shida kudhibiti harakati za mikono, miguu, na sehemu nyingine za mwili. Hali hii huathiri uwezo wa kukaa na kutembea.
Utindio wa ubongo wa aina ya Dyskinetic unajumuisha aina mbalimbali ambazo ni athetoid, choreoathetoid na dystonic. Harakati/mwendo huwa hazidhibitiki (uncontrolled movement), zinaweza kuwa polepole na za kujizungusha, au za ghafla na kurukaruka.
Mara nyingine uso na ulimi huathirika, jambo linaloleta changamoto kwenye kunyonya, kumeza na kuzungumza.
Toni ya misuli kwa watu/watoto hawa hubadilika mara kwa mara ambapo inaweza kuwa ngumu kupita kiasi au laini kupita kiasi, na mabadiliko haya huweza kutokea hata ndani ya siku moja.
3. Utindio wa Ubongo wa aina ya Ataxic
Aina hii huathiri usawazishaji na uratibu wa harakati (balance and movement control). Watu/watoto huweza kuwa hawana uthabiti wanapotembea, hupata shida kufanya harakati za haraka au zinazohitaji umakini mkubwa, kama vile kuandika. Pia, huwa na ugumu wa kudhibiti mikono au mikono inapojaribu kuchukua kitu.
4. Utindio wa ubongo wa aina Mchanganyiko (Mixed CP)
Watu wengine huonyesha dalili za aina zaidi ya moja ya utindio wa ubongo. Aina ya mchanganyiko inayopatikana sana ni spastic-dyskinetic CP (yaani utindio wa ubongo wa spastic na wa dyskinetic).
Nini husababisha Utindio wa Ubongo?
Utindio wa Ubongo (CP) husababishwa na ukuaji usio wa kawaida wa ubongo au kuumia kwa ubongo unaoendelea kukua, jambo linaloathiri uwezo wa mtoto kudhibiti misuli yake.
Kuna sababu kadhaa zinazoweza kuchangia matatizo haya.
Awali, watu walidhani kwamba utindio wa ubongo husababishwa hasa na upungufu wa oksijeni wakati wa kujifungua, lakini sasa wanasayansi wanaamini kuwa hali hiyo inachangia asilimia ndogo tu ya visa vya utindio wa ubongo.
Hivyo maendeleo yasiyo ya kawaida au majeraha ya ubongo yanatokea kabla ya kuzaliwa, wakati wa kuzaliwa, ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa, katika miaka ya awali ya maisha ya mtoto na wakati ubongo bado unaendelea kukua; hizi zote zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
I. Utindio wa ubongo wa kuzaliwa (Congenital CP)
Hii ni aina ya utindio wa ubongo inayotokea kutokana na matatizo ya ubongo kabla ya kuzaliwa au wakati wa kuzaliwa. Asilimia kubwa ya utindio wa ubongo (takriban 85% hadi 90%) ni ya kuzaliwa.
Mara nyingi, sababu halisi ya kutokea kwa hali hii haijulikani.
II. Utindio wa ubongo wa baada ya kuzaliwa (Acquired CP)
Idadi ndogo ya visa vya utindio wa ubongo husababishwa na matatizo ya ubongo yanayotokea zaidi ya siku 28 baada ya kuzaliwa.
Utindio wa ubongo wa aina hii huambatana mara nyingi na maambukizi ya ubongo (kama vile meningitis) pamoja na majeraha ya kichwa.
Kwa ujumla visababishi vikuu vya utindio wa ubongo ni kukosa hewa (oksijeni) wakati wa kuzaliwa, kuzaliwa kabla ya muda (njiti), manjano kali kwa mtoto mchanga, majeraha ya kichwa katika miaka ya awali pamoja na homa ya uti wa mgongo au degedege.
Dalili za Utindio wa Ubongo kwa Watoto
Dalili zake hutofautiana sana kwa sababu kuna aina nyingi na viwango tofauti vya ulemavu. Ishara kuu kwamba mtoto huenda ana utindio wa ubongo ni kuchelewa kufikia hatua muhimu za ukuaji (kama vile kujigeuza, kukaa, kusimama, au kutembea).
Ni muhimu kutambua kwamba watoto wengine wasiokuwa na utindio wa ubongo pia wanaweza kuwa na baadhi ya dalili hizi hivyo ni vema kuwaona wataalamu wa afya au kumpeleka mtoto hospitalini pindi uonapo dalili hizi.
Zifuatazo ni dalili za utindio wa ubongo:
Kwa Mtoto Mchanga Chini ya Miezi 6
- Kushindwa kukaza kichwa
- Mwili wake huhisi kuwa mgumu.
- Mwili wake huhisi kuwa legevu kupita kiasi.
- Unapombeba kwenye mikono yako, huonekana kama anakunjua mgongo na shingo kupita kiasi, daima akionekana kama anataka kujitoa kutoka kwako.
- Unapombeba juu, miguu yake hujikunja na kukatiza au kusulubiana.
Kwa Mtoto Zaidi ya Miezi 6
- Hawezi kujigeuza upande wowote.
- Hawezi kuleta mikono yake pamoja.
- Huwa na ugumu wa kupeleka mikono yake mdomoni.
- Anatoa mkono mmoja tu huku mwingine ukiwa umefungwa kwa ngumi.
Kwa Mtoto Zaidi ya Miezi 10
- Anacheza au kutambaa kwa namna isiyo ya kawaida, akijisukuma kwa mkono na mguu mmoja huku akiburuta mkono na mguu wa upande mwingine.
- Anajisogeza akitumia matako au anaruka kwa magoti bila kutambaa kwa kutumia mikono na miguu yote minne.
Kumbuka: Ni muhimu kumtaarifu mtaalam wa afya ukiona mojawapo ya dalili hizi kwa mwanao.
Matibabu ya Utindio wa Ubongo
Hakuna tiba kamili ya utindio wa ubongo (CP), lakini utambuzi wa mapema na matibabu ya haraka vinaweza kuboresha maisha ya watu wenye hali hii. Ni muhimu kuanza mpango wa matibabu haraka iwezekanavyo.
Baada ya mtoto kugundulika kuwa na utindio wa ubongo, kikundi cha wataalamu wa afya hufanya kazi kwa pamoja na mtoto na familia yake ili kuandaa mpango wa kumsaidia mtoto kufikia uwezo wake kamili, ambapo matibabu yanaweza kuwa:
- Dawa za kifafa au kukabiliana na degedege
- Upasuaji
- Tiba ya viungo (Physiotherapy)
- Tiba ya kazi (Occupational therapy)
- Tiba ya kusema na mawasiliano (speech therapy)
- Vifaa saidizi kama kiti mwendo (CP wheelchair)
- Bila kusahau msaada wa familia na mapenzi ya dhati huongeza matumaini kwa mtoto mwenye utindio wa ubongo
Mwisho
Kabla ya kuchagua mpango wa matibabu, ni muhimu kuzungumza na daktari wa mtoto ili kuelewa kikamilifu faida na hatari zinazoweza kutokea.
Lakini pia ni muhimu jamii kutambua kuwa utindio wa ubongo si ugonjwa wa kuambukiza, na watoto wenye hali hii wanaweza kufikia mafanikio makubwa endapo watapatiwa msaada sahihi.
Kwa mahitaji ya vifaa tiba vitakavyoweza kumsaidia mtoto wako mwenye changamoto hii ya CP, usisite kuwasiliana nasi kupitia simu namba: +255 767 226 702

Physiotherapist Officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
