Katika jamii kumekuwa na fikra potofu kuhusiana na maumivu ya shingo, wengi wakiamini hili ni tatizo la wazee tu lakini pia wengi huamini kuwa maumivu ya shingo ni kawaida kadri umri unavyozidi kuongezeka.
Ukweli ni kwamba maumivu ya shingo yanaweza kuathiri mtu wa umri wowote lakini wazee wanaweza kuathirika zaidi na aina fulani ya maumivu ya shingo kutokana na mabadiliko katika pingili za uti wa mgongo.
Lakini sio swala linalohusiana na umri pekee, zipo zababu nyingi zinazopelekea maumivu ya shingo na kwa bahati nzuri sababu hizo zinaweza zikashughulikiwa kwa kawaida endapo zitapatiwa uchunguzi na matibabu sahihi.
Kwa kuzingatia kwamba kutambua chanzo cha maumivu ni hatua ya kwanza katika kupata tiba sahihi na kupunguza madhara yanayoweza kuendelea kwa muda mrefu. Katika makala hii nitaelezea sababu zinazopelekea maumivu ya shingo, dalili zake na tiba sahihi ya maumivu ya shingo.
Nini hasa kinapelekea maumivu ya shingo?
Kuna sababu mbalimbali ambazo hupelekea kuhisi maumivu ya shingo. Maumivu hayo huweza kutokea kama zao la tabia, shughuli za kila siku au hali ya ugonjwa wa muda mrefu; nazo ni pamoja na
- Mikakamao ya misuli ya shingo
- Homa yabisi (Arthritis kwa mara nyingi osteoarthritis)
- Kupasuka au kuharibika kwa diski/pingili za uti wa mgongo
- Mkao mbaya ambao kwa kiasi kikubwa unawaathri watumiaji wa komputa katika maeneo ya kazi na watumiaji wa simu ya mkononi kwa muda mrefu.
- Kufanya kazi zinazoweka uzito shingoni na mabegani kama vile kubeba vitu vizito kichwani na mabegani kunachangia maumivu ya shingo.
- Ajali za barabarani, michezo, au kazi zinazosababisha shingo kukunjuka vibaya zinaweza kusababisha maumivu makali ya shingo.
- Mgandamizo au shinikizo la neva/mishipa ya fahamu inayopitia shingoni inaweza kusongwa na diski za uti wa mgongo – hali inayosababisha maumivu makali ya kichwa, shingo, kichwa, mabega na hata mikononi.
- Baadhi ya tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa kuna mambo ya kisaikolojia (kama vile msongo wa mawazo pamoja na matatizo ya usingizi) zinazochangia maumivu ya shingo.
Maumivu ya Shingo Yana Dalili Zipi?
- Ugumu wa kugeuza shingo kwa raha.
- Baadhi ya tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa kuna mambo ya kisaikolojia (kama vile msongo wa mawazo pamoja na matatizo ya usingizi) zinazochangia maumivu ya shingo.
- Maumivu ya kusambaa (radicular pain): Haya ni maumivu ambayo huenea hadi kwenye mabega, mikono, au kichwani. Mara nyingi hutoka kwa mvutano au mkazo wa misuli kwenye shingo.
- Kuhisi mvutano au mafundo kwenye misuli ya shingo.
- Ganzi katika mikono au mikono kutokana na mkandamizo wa mishipa ya fahamu shingoni.
- Mzunguko mdogo wa mwendo au maumivu na harakati za shingo.
Dalili za hatari zinazoambatana na maumivu ya shingo
Kwa watu wenye maumivu ya shingo, kuna dalili fulani ambazo zinapaswa kuzua wasiwasi. Hizi ni pamoja na:
- Kupoteza nguvu, hisia au ganzi katika mikono na miguu—huenda ikawa ishara ya uharibifu wa neva au mishipa ya fahamu.
- Homa
- Kutokwa na jasho usiku
- Maumivu ya kichwa
- Uchovu kupita kiasi au kuchanganyikiwa
- Maumivu ya kifua
- Kutokwa na jasho ghafla au ugumu wa kupumua
- Maumivu yanayosababishwa na shughuli au yanayoongezeka unapojitahidi
Zingatia: Ikiwa mtu ana dalili hizi, ni muhimu kutafuta msaada wa kitabibu haraka.
Tiba za Viungo (Fiziotherapia) kwa Maumivu ya Shingo
Tiba za viungo ni mojawapo ya matibabu ya maumivu ya shingo na ni muhimu sana katika kusaidia kuponya au kupunguza maumivu ya shingo.
Tiba hizi huhusisha mbinu mbalimbali za kutoa maumivu ya shingo ikiwa ni pamoja na kutibu kutokana na sababu iliyopelekea maumivu hayo.
Wataalamu wa tiba za viungo huchukua taarifa muhimu kwa mgonjwa wa shingo kabla ya kuanza kutoa matibabu lengo ikiwa ni kuhakikisha matibabu yanakwenda kutibu tatizo kwa kupambana na chanzo husika cha tatizo.
Tiba hii inahusisha:
- Kutoa elimu kwa mgonjwa juu ya tatizo, chanzo cha tatizo lake na namna tiba itakavyokwenda kumsaidia
- Mkao sahihi, mazoezi ya shingo, pamoja na mbinu kama vile tiba ya joto kupunguza mkazo wa misuli (heating pads), barafu kupunguza maumivu, na kichocheo cha umeme kama vile Transcutaneous electrical nerve stimulation (TENS) – kifaa ambacho husaidia kupunguza maumivu ya shingo.
- Mazoezi ya shingo na mbinu mbalimbali zinazolenga kuondoa ukakamau shingoni na hivyo kupunguza au kuondoa kabisa maumivu ya shingo.
- Mvutano (cervical traction machine), unaosimamiwa na Mtaalam wa tiba ya viungo, kifaa hiki hutumia uzani na puli, kunyoosha shingo polepole ili kutoa ahueni ya maumivu ya shingo – haswa kwa maumivu yatokanayo na kubanwa au kushinikizwa kwa mishipa ya fahamu inayotokea shingoni.
- Matumizi ya kifaa maalumu cha kuvaa shingoni kama kola (cervical collars), ambacho husaidia kuimarisha shingo na kupunguza maumivu yanayotokana na uharibifu wa viungo vya shingo.
- Pia matumizi ya kifaa kama mto wa shingo (cervical pillows), ambao ni mto maalumu unaotengenezwa kwa ajili ya kusaidia mkao sahihi wa kichwa na shingo unapolala. Mto huu husaidia kuzuia na kuondoa maumivu ya shingo yatokanayo na mikao isiyo sahihi.
Nini Kifanyike Kuzuia au Kujikinga na Maumivu ya Shingo?
Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili kuepukana na maumivu ya shingo, hasa katika maeneo ya kazi na ofisini.
- Dumisha mkao unaofaa wakati umekaa, umesimama, au ukitumia vifaa vya kidijitali kama komputa na simu za mkononi ili kupunguza mkazo kwenye misuli ya shingo.
- Tumia samani (viti na meza) zinashoshauriwa na wataalamu ambazo zitakufanya uwe katika mkao sahihi uwapo ofisini ukitizama komputa yako katika kiwango cha macho ili kuepuka kupinda kwa shingo.
- Chukua mapumziko mafupi ili kunyoosha shingo na mabega yako wakati wa saa ndefu za kazi au matumizi ya vifaa kama computer (desktop au laptop).
- Lala ukitumia mto wa kuunga mkono na uepuke kulala juu ya tumbo lako, kwani hii inaweza kusababisha shingo yako kujipinda isivyo kawaida.
- Imarisha misuli ya shingo na sehemu ya juu ya mgongo kwa kufanya mazoezi ya kawaida ili kuboresha unyumbulifu wa misuli ya shingo.
- Epuka kubeba mifuko mizito upande mmoja wa bega ili kuzuia usawa wa misuli ya shingo.
- Dhibiti msongo wa Mawazo kwa kutumia mbinu za utulivu kama kufanya mazoezi ya kutafakari (meditation) na mazoezi ya kujinyoosha misuli ya shingo,mabega na mgongo, kwani msongo wa Mawazo unafanya shingo kuwa ngumu na kuleta maumivu.
Kwa kuhitimisha…
Maumivu ya shingo ni hali inayoweza kuathiri ubora wa maisha yako; kufanya uchunguzi na kupata tiba sahihi mapema ni muhimu sana ili kuzuia kuongezeka kwa tatizo. Pia matibabu yake hutegemeana na sababu husika, hivyo kuna haja ya kuhusisha wataalam wa afya nje ya fiziotherapia pale inapohitajika.
Lakini pia kwa mahitaji ya vifaa tiba nilivyovielezea kwenye ‘Tiba ya Viungo’, unaweza kutembelea duka letu linalopatikana Sinza Mori, jengo la Azaria Plaza (ofisi na. 14), opposite na Kitambaa Cheupe Sinza.
Kama unapatikana nje ya mkoa wa Dar es Salaam, tupigie simu kwenye namba +255 767 226 702 tukufanyie delivery popote Tanzania.
Kwa taarifa zaidi kuhusu vifaa tiba vyetu vyote, tembelea tovuti yetu ya shop.abiteafya.com au Instagram yetu hapa.
An aspiring Physiotherapist officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
I have understood well.
Thank you very much for your article.