Ganzi ya miguu ni hali ya kukosa hisia au kuhisi kama kuchoma choma au sindano kwenye miguu, mara nyingi husababishwa na kugandamizwa kwa mishipa ya fahamu.
Kugandamizwa huku husababishwa na kuteleza kwa pingili za mgongo (disc herniation), kusagika kwa pingili za uti wa mgongo (degenerative disc diseases) na mikao isiyo sahihi kwa muda mrefu.
Lakini pia yapo matatizo mengine kama vile kisukari au mzunguko duni wa damu ambao pia hupelekea uwepo wa ganzi miguuni.
Hivyo kusumbuliwa na ganzi ni dalili inayoashiria moja ya matatizo hayo na tiba yake huwa ni kudhibiti chanzo cha tatizo.
Sasa iwapo umekuwa ukisumbuliwa na ganzi kwa muda mrefu na hujui nini cha kufanya, nakushauri kufata hatua zifuatazo ili kupatiwa usaidizi mapema:
- Muone mtaalamu wa Afya, kwani ganzi ya muda mrefu inahitaji uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini chanzo.
- Fanya mazoezi ya kunyoosha viungo (stretching) ambayo husaidia kuondoa mgandamizo kwenye mishipa ya fahamu (neva), hasa kwenye mgongo wa chini.
- Zingatia mkao wako kwa kuwa kukaa au kulala vibaya kwa muda mrefu kunaweza kuchangia ganzi miguuni, hata mikononi.
- Dhibiti magonjwa sugu, kama una kashkari, kiharusi (stroke), magonjwa ya mfumo wa fahamu (multiple sclerosis, peripheral neuropathy, carpal tunnel syndrome), upungufu wa Vitamini B12 na mengineyo, hakikisha yanadhibitiwa.
- Epuka kubeba mizigo mizito: Hii huongeza shinikizo kwenye uti wa mgongo na kupelekea ganzi.
ZINGATIA: Sio kila ganzi ya miguu ni dalili ya changamoto au shida fulani katika mgongo.
Mfano, binafsi nilishawahi kumuona Baba mmoja mwenye umri wa miaka 45 aliyeripoti kliniki akisumbuliwa na maumivu ya mgongo wa chini pamoja na ganzi miguuni.
Baada ya kumfanyia uchunguzi wa awali nikaomba akafanye vipimo zaidi ikiwemo kipimo cha sukari na mwishowe akabainika kuwa na tatizo la figo pamoja na kisukari, matatizo ambayo ndio yalikuwa yakipelekea dalili ya ganzi miguuni na hata maumivu ya mgongo.
Hivyo ni muhimu, kabla ya kufanya chochote, kumtembelea mtaalamu wa afya na kufanya uchunguzi wa afya yako pindi tu uonapo dalili isiyo ya kawaida mwilini, kwani kwa kufanya hivyo utapatiwa tiba sahihi mapema na hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea kwa athari zingine hapo baadae.
Mwisho
Ganzi huweza kutokea sehemu zingine za mwili kama vile mikono, mdomo, na kadhalika na yote hayo huhitaji uchunguzi ipasavyo.
Ganzi ya muda mrefu au mara kwa mara si jambo la kubeza. Ikiwa inaendelea kwa zaidi ya siku kadhaa au inaambatana na udhaifu wa misuli, usisite kuwaona wataalamu wa afya mapema au mtaalamu wa tiba ya viungo (physiotherapist) kwa uchunguzi zaidi.

Physiotherapist Officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
