Kiharusi ni hali ya dharura ya kiafya inayotokea pale ambapo damu inashindwa kufika kwenye sehemu fulani ya ubongo, ambayo hutokana na kuziba kwa mshipa wa damu au kupasuka kwa mshipa ya damu inayopeleka damu kwenye ubongo.
Matokeo yake ni kuharibika kwa seli za ubongo, jambo linaloweza kusababisha kupoteza uwezo wa kuzungumza, kutembea, au hata kufanya shughuli za kila siku.
Kutokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hivi karibuni zinaonyesha kwamba kila mwaka watu milioni 15 duniani hupata kiharusi. Kati yao, milioni 5 hufariki na milioni 5 nyingine hubakia na ulemavu wa kudumu, jambo linaloelemea familia na jamii kwa ujumla.
Pia kiharusi kinawapata sana wazee huku kikitokea mara chache kwa walio chini ya miaka 40 na kikitokea mara nyingi sababu huwa ni shinikizo la juu la damu. Aidha, takriban 8% ya watoto wenye ugonjwa wa seli mundu hupata kiharusi.
Shinikizo la juu la damu na matumizi ya tumbaku ni sababu kuu zinazoweza kudhibitiwa kwani kwa kila watu 10 wanaofariki kwa kiharusi, wanne wangeweza kuokolewa iwapo shinikizo lao la damu lingedhibitiwa.
Kwa walio chini ya miaka 65, 40% ya vifo vya kiharusi vinahusiana na uvutaji sigara. Mambo mengine yanayoongeza hatari ni pamoja na matatizo ya mapigo ya moyo (atrial fibrillation), kushindwa kwa moyo kufanya kazi, na mshtuko wa moyo.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hili nimeona kuna haja ya kuongeza ufahamu kwa jamii juu ya tatizo hili. Soma makala hii hadi mwisho, kuna kitu utajifunza.
Aina za Kiharusi
Ubongo unafanya kazi kwa namna ambapo upande wa kulia wa ubongo unaratibu mikono na miguu ya upande wa kushoto, na ubongo wa kushoto unaratibu mikono na miguu ya kulia.
Kiharusi hugawanywa katika makundi mawili kulingana na mchakato wa ugonjwa:
- Kiharusi cha ischemic (Ischaemic stroke): Husababishwa na kuziba kwa mshipa mkubwa wa ubongo kutokana na kuganda kwa damu, na ni aina maarufu zaidi ya kiharusi ikihusisha takriban 80-85% ya wagonjwa wenye kiharusi.
- Kiharusi cha hemorrhagic (hemorrhagic stroke): Hutokea pale mishipa ya damu inapopasuka na damu kuvuja ndani au nje ya ubongo. Sababu zake ni pamoja na shinikizo la damu, tiba ya kupunguza kuganda kwa damu, majeraha, au uzee. Aina hii ya kiharusi huathiri 15–20% ya wagonjwa.
- Shambulio la muda mfupi la iskemia (Mini Stroke/Transient Ischaemic Attack – TIA), ambapo dalili hupotea ndani ya saa 24. Aina hii ina matokeo bora zaidi, ikifuatiwa na kiharusi cha ischemic kisha kiharusi cha hemorrhagic – ambacho ni hatari zaidi kuliko aina zote.
Dalili za hatari za kiharusi ambazo ni vema kila msomaji wa makala hii akazifahamu ili kuchukua hatua mapema ni pamoja na:
- Kupooza ghafla upande mmoja wa mwili (uso, mkono au mguu)
- Kuchanganyikiwa au kushindwa kuzungumza au kuelewa maneno
- Kupoteza uwezo wa kuona kwa jicho moja au yote mawili
- Kizunguzungu, kutembea kwa shida au kupoteza usawa
- Maumivu makali ya kichwa yasiyo ya kawaida yanayoanza ghafla bila sababu dhahiri
Zingatia: Dalili hizi zinaweza kutokea ghafla na ni dharura ya kitabibu. Mara tu ukihisi dalili hizo wapigie ambulance mapema au nenda hospitali iliyopo karibu nawe.
Tiba ya Kiharusi
Athari za kiharusi huweza kuwa za muda mrefu, huduma ya haraka na utengamao wa muda mrefu ni muhimu sana kwa mgonjwa.
Utengamao kwa wagonjwa wa kiharusi unahusisha tiba mbalimbali ikiwemo tiba ya dawa, tiba ya kisaikolojia, tiba ya usemi (speech therapy), tiba ya kazi (occupational therapy) pamoja na tiba ya mazoezi (physiotherapy).
Hivyo huduma kwa mgonjwa wa kiharusi haiishii tu kwenye matibabu ya awali hospitalini, bali huendelea kwa muda mrefu kupitia tiba hizo.
Kama nilivyo ainisha hapo awali kwamba nitaelezea zaidi ni kwa namna gani mazoezi tiba humsaidia mgonjwa wa kiharusi ambapo malengo makuu ya tiba hii ni:
- Kurejeshea mgonjwa uwezo wa kufanya shughuli za kila siku kama kula, kuoga, na kutembea.
- Kupunguzia ulemavu wa muda mrefu na hatari ya matatizo ya kiafya yanayoweza kuambatana.
- Kuboresha ubora wa maisha ya mgonjwa.
- Kusaidia mgonjwa kujitegemea na kuishi kwa heshima.
Tiba hii inahusisha mbinu zifuatazo:
Makundi makuu ya tiba za physiotherapy kwa mgonjwa wa kiharusi ni haya yafuatayo:
1. Tiba ya Mazoezi ya Mwili (Therapeutic Exercises)
Husaidia kurejesha nguvu za misuli, kuboresha mjongeo wa viungo, na kurudisha uwezo wa kufanya kazi za kila siku. Hujumuisha mazoezi ya kunyoosha, kuimarisha misuli, na kuongeza usawa wa mwili.
2. Mazoezi ya Usawa na Mjongeo (Balance and Gait Training)
Husaidia mgonjwa kujifunza kutembea tena, kuboresha usawa, na kupunguza hatari ya kuanguka. Hutumia vifaa kama parallel bars, walking aids (mf. vijiti, walker), au fimbo yenye miguu minne kwa usaidizi zaidi (quad cane).
3. Tiba ya Mfumo wa Fahamu (Neurodevelopmental Therapy – NDT)
Huwalenga wagonjwa wa kiharusi kwa kusaidia kurejesha mwendo sahihi na kuondoa mienendo mibaya (abnormal movement patterns).
4. Tiba ya Utendaji wa Kila Siku (Functional Training)
Husaidia wagonjwa kujifunza tena kufanya kazi kama kuvaa, kula, kuoga na kadhalika. Lengo ni kumwezesha mgonjwa kujitegemea zaidi.
5. Tiba ya Vifaa Saidizi (Assistive Devices Training)
Mgonjwa hufundishwa kutumia vifaa saidizi (braces, splints, au orthotics) kusaidia harakati au kulinda viungo mfano Arm sling ili kushikilia mkono uliodhoofika, shoulder support ili kuzuia mkono usishuke kwa wagonjwa wenye hemiplegia pamoja na kiti mwendo (wheelchair) endapo mgonjwa hawezi kutembea kabisa.
6. Tiba ya Maumivu (Pain Management)
Hujumuisha matumizi ya vifaa tiba vya mwili kama Transcutaneous Electrical Nerve Sitimulation (TENS), kifaa ambacho hutumia umeme mdogo kupunguza maumivu, heating pads na cold packs ambazo hutolewa kwa umakini kutokana na hali ya mgonjwa.
Mwisho
Huduma bora kwa mgonjwa wa kiharusi inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa afya (daktari, mfiziotherapia, mtaalamu wa usemi, mtaalamu wa tiba kazi) na familia.
Familia pia inapaswa kufundishwa namna ya kumsaidia mgonjwa nyumbani, kumtia moyo, na kuhakikisha mazingira yanamfaa mgonjwa.
Kiharusi ni changamoto kubwa ya kiafya, lakini si mwisho wa maisha. Kupitia tiba na huduma sahihi mgonjwa anaweza kurejea katika hali ya kawaida na kuishi kwa heshima. Ushirikiano wa wataalamu na familia ni msingi wa mafanikio ya ukarabati.

Physiotherapist Officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
