Faida za Mazoezi Tiba Kwenye Maumivu Sugu ya Viungo

Mazoezi tiba (Therapeutic exercises) ni miongoni mwa tiba ambayo hutumiwa na wataalamu wa tiba za viungo kutibu magonjwa mbalimbali.

Tiba hii ni sehemu muhimu ya matibabu kwa watu wanaosumbuliwa na maumivu sugu kama ya mgongo, viungo, shingo, mabega, na magoti.

Maumivu haya, mara nyingi, hutokana na hali kama vile homa yabisi (arthritis), matatizo ya pingili za mgongo (disc problems), majeraha ya tishu (fibromyalgia), au matatizo ya mkao wa mwili.

Tiba hii ikitumika ipasavyo na wataalam wa tiba ya viungo, ikiwa pekeake au ikiambatanishwa na tiba nyingine za viungo, hutoa matokeo mazuri sana kwa mgonjwa. Inajumuisha faida zifuatazo:

1. Kupunguza maumivu

Mazoezi husaidia kupunguza maumivu kwa kuongeza damu kwenda kwenye misuli na tishu zilizoathirika. Hii huongeza virutubisho na oksijeni hivyo kusaidia kuondoa sumu au uchafu uliosababisha maumivu.

2. Kuongeza uwezo wa kutembea na kufanya shughuli

Mazoezi husaidia kurudisha au kuboresha uwezo wa mwili kufanya kazi za kila siku kama kutembea, kuinama, kukaa au kuinua vitu. Hii huongeza uhuru wa mgonjwa na kumfanya kuwa huru zaidi bila msaada.

3. Kuimarisha misuli na viungo

Kwa watu wenye maumivu sugu, misuli hushambuliwa kwa kudhoofika kutokana na kutotumika. Mazoezi huimarisha misuli, kuzuia udhaifu, na kusaidia kupunguza mzigo kwenye viungo vya mwili.

4. Kuboresha mzunguko wa damu na utulivu

Mazoezi huongeza mzunguko wa damu mwilini ambao husaidia uponyaji wa tishu. Pia huchochea utoaji wa homoni (endorphins) ambazo hupunguza maumivu na kuongeza hali ya furaha.

5. Kurekebisha mkao wa mwili (posture)

Maumivu sugu mara nyingi huhusishwa na mkao mbaya. Mazoezi husaidia kurekebisha mkao wa mwili na kupunguza mzigo usio wa lazima kwenye misuli na mifupa.

6. Kupunguza utegemezi wa dawa

Wagonjwa wengi wa maumivu sugu hutegemea dawa kwa muda mrefu ambazo zinaweza kuwa na madhara ya muda mrefu. Mazoezi ni njia mbadala isiyo ya dawa ya kudhibiti na kutibu maumivu.

7. Kuongeza ujasiri na afya ya akili

Maumivu ya muda mrefu huathiri pia afya ya akili. Kufanya mazoezi mara kwa mara huongeza imani ya mtu kwa mwili wake, hupunguza msongo wa mawazo na huchangia hali ya utulivu wa kisaikolojia.

Mazoezi tiba yana madhara yoyote?

Licha ya faida mbalimbali za mazoezi tiba, tunapasawa pia kutambua kwamba endapo mazoezi tiba yatatolewa bila kufata ushauri na uangalizi wa mtaalamu wa mazoezi tiba yanaweza kupelekea hasara na pengine hatari katika afya ya mgonjwa.

Baadhi ya athari na madhara ambayo yamekuwa yakiwapata wagonjwa wanaofanya mazoezi tiba bila kufata ushauri wa wataalamu ni pamoja na kufeli kwa figo, kupanda kwa shinikizo la damu na kusababisha maumivu au majeraha zaidi katika eneo husika linalopatiwa matibabu.

Hivyo ni muhimu kushiriki mazoezi tiba huku ukipatiwa ushauri na uangalizi kutoka kwa mtaalam wa tiba ya viungo bila kusahau kumaliza mpango wa matibabu utakaopangiwa ili kurejea katika hali yako ya kawaida kwa mapema.

Je, mazoezi tiba yanaweza kutolewa nyumbani?

Ndio, mazoezi tiba yanaweza yakatolewa kwa mgonjwa akiwa nyumbani, na hii imekuwa ikifanywa zaidi kwa wagonjwa ambao wanahitaji huduma hizi kwa muda mrefu ikiwemo wagonjwa wa kiharusi na magonjwa hadimu ambapo kwa kiasi kikubwa inawapunguzia wagonjwa hawa ghalama za usafiri mara kwa mara kufata huduma za mazoezi tiba hospitalini.

Hivyo, ili kushiriki mazoezi tiba ukiwa nyumbani ni vema kuzingatia kwamba huduma hizi zinatolewa na mtaalamu mwenye ujuzi na pia kuwe na vifaa vya kufanyia mazoezi ambavyo vitatakiwa viwepo baada ya mtaalamu wa tiba ya viungo kushauri.

Je, mazoezi tiba yanaweza kutolewa kwa njia ya mtandao?

Ndio, katika nchi zilizoendelea tayari zimeshaanza kufanikisha utoaji wa huduma za mazoezi tiba kwa njia ya mtandao (telerehabilitation/digital rehabilitation); kupitia njia hii mgonjwa anaweza akashiriki tiba ya mazoezi kwa kutumia programu za mtandao na akili bandia (AI).

Nchini Tanzania tayari wataalam wa huduma za utengamao kwa kushirikiana na wabunifu, wadau mbalimbali pamoja na Wizara ya Afya wameanza utekelezaji chini ya mpango uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) wa “Ajenda ya huduma za utengamao 2030” kukabiliana na pengo la teknolojia ili kuhakikisha huduma hii itakapoanza iongeze upatikanaji wa huduma za utengamao ikiwemo mazoezi tiba kwa njia ya mtandao ili kurahisisha upatikanaji na unafuu wa huduma hii.

Hitimisho

Mazoezi tiba ni suluhisho salama, la muda mrefu na lenye tija kwa watu wanaokabiliwa na maumivu sugu ya viungo. Kwa kushirikiana na mtaalamu wa fiziotherapia, mgonjwa atapata mpango bora wa mazoezi kulingana na hali yake binafsi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *