Maumivu ya kisigino ni tatizo linaloathiri mamilioni ya watu duniani, ikiwa chanzo cha usumbufu mkubwa katika maisha ya kila siku.
Maumivu haya yanaweza kuwa kikwazo kikubwa katika utendaji wa kawaida wa mwili, hasa kwa wale wanaotegemea miguu kwa shughuli za kila siku kama kutembea, kusimama kazini au kushiriki michezo.
Hata hivyo, maumivu ya kisigino ni hali inayoweza kuathiri watu wa rika zote na mara nyingi ni matokeo ya matumizi ya kisigino kupita kiasi, jeraha, au hali ya kiafya ya msingi.
Hutokea mara nyingi sehemu ya chini au nyuma ya kisigino na yanaweza kuwa maumivu madogo au makali.
Lakini pia maumivu ya kisigino huambatana na dalili nyingine kama ugumu wa eneo la kisigino na unyayo hasa wakati wa kutembea, uvimbe na wekundu katika eneo hilo pamoja na ongezeko la joto katika eneo la kisigino.
Aina za Maumivu ya Kisigino
Maumivu haya yamegawanyika kulingana na eneo yanapotokea ambapo kuna:
I. Maumivu chini ya kisigino (plantar): yanaathiri sehemu inayogusa ardhi inapokanyaga.
Plantar fasciitis ndio sababu kuu ya aina hii ya maumivu ya kisigino; husababishwa na kuvimba kwa kiwambo cha nyuzi kinachounganisha kisigino na vidole. Maumivu haya huwa makali zaidi asubuhi.
II. Maumivu nyuma ya kisigino (posterior): Hutokea sehemu inayounganisha kisigino na misuli ya nyuma ya mguu.
Kwa kiasi kikubwa huchangiwa na mifupa ya kisigino, heel spurs, ambapo hutokana na mikusanyiko ya madini ya kalsiamu inayosababisha ukuaji wa mfupa usio wa kawaida na hivyo kupelekea maumivu makali sana eneo la kisigino.
Nini Husababisha Maumivu ya Kisigino?
Zifuatazo ni sababu zinazoweza kupelekea maumivu ya kisigino, ambapo nyingi zinamajina ya kitaalamu lakini kwenye makala hii nimejitahidi kutoa maelezo ya kutosheleza ili wewe msomaji uelewe zaidi:
1. Jeraha la jiwe: Hutokea baada ya kukanyaga kitu kigumu, na kusababisha maumivu ya ndani ya kisigino.
2. Mifupa ya kisigino (heel spurs): Ambapo hutokana na mikusanyiko ya madini ya kalsiamu inayosababisha ukuaji wa mfupa usio wa kawaida na hivyo kupelekea maumivu makali sana eneo la kisigino.
3. Hali ya kushinikizwa kwa mishipa ya fahamu ya nyuma ya mguu (Tarsal tunnel syndrome): Hali ambayo husababisha ganzi na maumivu ya kuchomachoma.
4. Kuvimba kwa tishu zinazounganisha misuli ya nyuma ya mguu na kisigino (Achilles tendonitis), mara nyingi kutokana na mazoezi kupita kiasi.
5. Maumivu yanayotokana na kuvimba kwa kiwango cha majimaji kinachopatikana kati ya kisigino na tendoni ya Achilles (Bursitis).
Husababishwa na viatu vyenye kisigino kirefu vinaposugua kisigino na kusababisha uvimbe hali ijulikanayo kitaalamu kama Haglund’s deformity.
Maumivu ya Kisigino Yana Matibabu?
Ndio! Matibabu yanategemea sababu na ukali wa maumivu, pamoja na hali yako ya afya kwa ujumla.
Matibabu yake yanaweza yakawa kwa kutumia dawa, upasuaji na tiba za viungo au fiziotherapia. Lakini makala hii itaeleza ni kwa namna gani mgongwa wa maumivu ya kisigino anavyoweza kunufaika na tiba za fiziotherapia.
1. Elimu kwa mgonjwa juu ya chanzo na matibabu sahihi ya tatizo lake. Lakini pia elimu juu ya tiba itakayozuia maumivu yasiendelee au tatizo lisiongezeke kama kupumzika na kubadilisha shughuli pindi maumivu yanapozidi kwa maana ya kusitisha shughuli kama kukimbia ama kusimama kwa muda mrefu.
Pia kuvaa viatu vinavyotoa msaada mzuri, usaidizi wa kisigino na vinavyolingana vyema vinaweza kupunguza shinikizo kwenye kisigino. Vingirizi vya visigino au pedi za visigino zinaweza kutoa msaada wa ziada.
2. Tiba ya barafu: Kuweka barafu kwenye kisigino kwa dakika 15-20 mara kadhaa kwa siku kunaweza kusaidia kupunguza uvimbe na maumivu.
3. Mazoezi tiba
Mazoezi maalumu yanayolenga kunyoosha tendoni ya Achilles, misuli ya paja, na plantar fascia yanaweza kuboresha unyumbufu na kupunguza maumivu ya kisigino cha mguu.
Mazoezi haya huongozwa na mtaalamu wa viungo, physiotherapist.
ZINGATIA: Matumizi ya barafu, na mazoezi ya kujinyoosha ni hatua zinazohitaji maelezo thabiti kutoka kwa mtaalam wa afya ili kuepuka athari zake hapo baadae.
4. Matumizi ya kifaa tiba (Splinti za usiku)
Kuvaa kifaa cha kunyoosha mguu usiku kunaweza kuweka mguu katika nafasi iliyonyoshwa, kupunguza maumivu ya asubuhi yanayohusiana na hali kama maumivu ya kisigino aina ya plantar fasciitis.
Pia matumizi ya vifaa tiba kama Heel Cushion na Silicone Insole ni muhimu kwenye kupunguza maumivu ya visigino; unaweza kuvivaa ukiwa kwenye mizunguko yako ya kila siku.
5. Tiba ya mawimbi ya mshtuko (Shockwave therapy)
Tiba hii ya mawimbi ya sauti husaidia uponyaji wa tishu laini, kama vile plantar fascia na hivyo kupunguza maumivu au kuondoa kabisa maumivu.
Nifanye Nini Ili Kuepuka Maumivu ya Kisigino?
- Vaa viatu vyenye msaada bora wa arch na kisigino, hasa ikiwa unatumia muda mwingi kusimama, kutembea, au kushiriki shughuli za michezo.
- Epuka shughuli zinazochosha miguu ghafla
- Nyoosha misuli mara kwa mara: Kunyoosha tendoni ya Achilles, misuli ya paja, na plantar fascia kunaweza kusaidia kuzuia ukakamavu unaosababisha maumivu ya kisigino
- Dhibiti uzito wa mwili wako kwani kuwa na uzito wa juu kunaweza kuongeza shinikizo kwenye kisigino, na kuongeza hatari ya maumivu na majeraha.
- Tumia visaidizi vya viatu hasa kama una miguu yenye matatizo ya kimuundo.
Mwisho
Maumivu ya kisigino yanaweza kudhibitiwa kwa urahisi iwapo utatambua dalili mapema na kuchukua hatua stahiki.
Iwapo maumivu haya yanadumu kwa muda mrefu au yanazidi kuwa makali, usisite kuonana na wataalamu wa afya kwa uchunguzi, tiba na ushauri sahihi ikizingatiwa kwamba matokeo ya matibabu ya maumivu hayo huweza kuwa maridhawa endapo kama chanzo cha maumivu kitajulikana na kutibiwa pale inapowezekana.
Pia, kuna haja ya kuhusisha wataalam wa afya tofauti tofauti kulingana na dalili zitakazoambatana na maumivu hayo au tatizo asilia lililogundulika.

Physiotherapist Officer (PTO), passionate about transforming the community through education, research and public health advocacy.
