Tiba ya Maumivu ya Mfupa wa Mkia wa Uti wa Mgongo

Matibabu ya tatizo hili yanahusisha tiba mbalimbali ikiwamo dawa kwa ajili ya kuondoa maumivu au ugonjwa unaopelekea maumivu, tiba ya viungo (physiotherapy) na muda mwingine huhitaji upasuaji kutibu tatizo.

Hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi kwa makini ili kujua chanzo cha tatizo kwa lengo la kupata huduma au tiba sahihi kwa mgonjwa.

Lakini kabla sijaendelea, naomba ukaptie makala yangu ya “Visababishi na Dalili za Maumivu ya Mfupa wa Uti wa Mgongo” ili twende sawa kwenye makala hii.

So katika makala hii nitajikita katika kuelezea ni kwa namna gani tiba ya viungo inaweza kutibu tatizo hili. 

Kwa kutumia mbinu mbalimbali, tiba ya viungo husaidia sana kupunguza maumivu ya mkia wa uti wa mgongo. Matibabu ya physiotherapy hutoa nafuu ya haraka huku yakifanya kazi kwenye eneo la mkia kwa ajili ya uponyaji wa muda mrefu.

1. Elimu kwa mgonjwa juu ya chanzo na tiba sahihi ya tatizo lake

Ambapo mtaalamu wa fiziotherapia hutoa elimu juu ya mtindo sahihi wa maisha kama vile lishe bora na umuhimu wa mazoezi ya viungo katika kukabiliana na uzito mkubwa.  

Hii ni kwasababu uzito uliopita kiasi umeonekana kuwa chanzo cha magongwa mengi na mara nyingi umekuwa ni chanzo cha kuleta matokeo mabaya (poor prognosis) kwa wagonjwa wanaoendelea na matibabu.

2. Tiba kwa kutumia vifaa vya umeme (electrotherapy)

Vifaa vya umeme kama TENS (Transcutaneous Electrical Nerve Stimulation) husaidi sana kuondoa maumivu ya mkia wa mgongo kwa kutumia umeme mdogo kupitia ngozi ili kupunguza maumivu; imeonekana kuwa na mafanikio makubwa kwa wagonjwa wa coccydynia. 

3. Mazoezi ya misuli ya sakafu ya kiuno (pelvic floor muscles) na mazoezi ya mgongo 

Hasa husaidia wagonjwa wenye maumivu ya misuli iliyoko karibu na mkia wa uti wa mgongo. Mazoezi ya kulegeza misuli ya pelvic floor husaidia kuweka mkia katika mpangilio bora, jambo linalosaidia kupunguza maumivu wakati wa kukojoa au kujisaidia.

Lakini pia mazoezi ya mgongo husaidia kunyosha na kuimarisha misuli ya eneo hilo ili kuleta utulivu na kupunguza maumivu. 

4. Mikao sahihi kwa kutumia vifaa tiba mbalimbali

Tiba nyingine na muhimu zaidi ni kutoa elimu kuhusu mkao sahihi wa mwili. Mtaalamu wa physiotherapy hukufundisha juu ya kurekebisha mkao pale unapoketi kwa kuketi ukiwa umesimama zaidi kwenye kiti kigumu.  

Mkao mzuri wa kuketi huhakikisha uzito hauwekwi kwenye mfupa wa mkia bali unasambazwa kwenye sehemu za chini za nyonga na mapaja. Wagonjwa wanashauriwa kuepuka mikao au mienendo yoyote ambayo inaweza kuendeleza au kuongeza maumivu yao. 

Hivyo, wataalamu wa tiba ya viungo hupendekeza matumizi ya mito maalum. Mito hii inaitwa Coccyx pillows (au Almohada coccyx), husaidia kupunguza shinikizo kwenye mfupa wa mkia wakati wa kuketi.  

Inapatikana Abite Nyumbani, tembelea kurasa yao ya Instagram “hapa” kwa taarifa zaidi.

Mito yenye umbo la duara, maarufu kama round ring pillow, pia inaweza kutumika. Hata hivyo, mito ya duara inaweza kuongeza shinikizo kwenye mfupa wa mkia, lakini ina faida zaidi kwa maumivu ya sehemu ya haja kubwa.  

Matumizi ya mito hii yanaweza kupendekezwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8. Ingawa hupendekezwa mara kwa mara, matokeo ya matibabu ya mapendekezo haya ya kawaida bado hayajathibitishwa kwenye tafiti za kitaalamu

Hitimisho

Kwa bahati nzuri, kesi nyingi za maumivu ya mkia wa mgongo zinaweza kutibiwa bila upasuaji kwa kutambua chanzo na kutumia tiba sahihi mfano matumizi ya mito ya kukalia na kurekebisha mkao inaweza kutibu tatizo hili; pia kama mbinu ya kujikinga na tatizo hili. 

 Hivyo iwapo unasumbuliwa na tatizo la maumivu ya kudumu ya mkia wa mgongo, wasiliana na mtaalamu wa afya kwa tathmini na ushauri.

Ukiwa na msaada sahihi, inawezekana kupona kabisa tatizo hili. Pia kuna haja ya kuhusisha wataalamu wengine wa afya pale inapohitajika. 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *