“Mgongo Ukikataa, Mwili Mzima Unalia”

Maumivu ya mgongo wa chini ni tatizo kubwa la afya kwenye jamii nyingi na ndio linaloongoza kwa kusababisha ulemavu duniani. Kutokana na takwimu za shirika la afya duniani (WHO) za hivi karibuni, inakadiriwa kuwa watu milioni 619 wanaishi na maumivu ya mgongo wa chini.

Pia inakadiriwa kuwa idadi ya visa itaongezeka hadi kufikia milioni 843 ifikapo mwaka 2050. Changamoto hii inaathiri watu wengi lakini elimu kuhusu dalili, visababishi vyake pamoja na njia za kuutibu bado imekua lugha ngeni kwenye jamii zetu.

Kupitia makala hii utafahamu nini husababisha maumivu ya mgongo, dalili zake pamoja na matibabu.

Maumivu ya mgongo wa chini ni maumivu yanayotokea kati ya ukingo wa chini wa mbavu na makalio.  Maumivu haya yanaweza kudumu kwa muda mfupi (wiki mbili hadi nne), muda wa kati (mwezi mmoja hadi mitatu), au kwa muda mrefu (ni maumivu sugu ambayo hudumu zaidi ya miezi mitatu).  

Maumivu ya mgongo wa chini yanaweza kumpata mtu wa umri wowote ikiwemo watoto, vijana na wazee huku umri kuanzia miaka 50 had 55 ukiongoza kuwa na visa vingi vya tatizo hili; huku wanawake wakiathrika zaidi ukilinganisha na wanaume.

Low back pain causes and treatment

Yanapompata mtu hupelekea ugumu wakati wa kugeuza mgongo  na yanaweza kuathiri ubora wa maisha na afya ya akili, lakini pia yanaweza kupunguza uwezo wa kufanya kazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kifamilia na kijamii. 

Nini Husababisha Maumivu ya Mgongo wa Chini?

  1. Mikao mibaya ya mwili 
    Kukaa au kusimama kwa muda mrefu kwa mkao usio sahihi, kama vile kujikunja mbele au kuegemea upande mmoja, huongeza mzigo kwa misuli ya mgongo. Hali hii husababisha kukakamaa kwa misuli ya mgongo hivyo kusababisha maumivu.

Lakini pia mkao mbaya huweka shinikizo lisilo la lazima kwenye uti wa mgongo na pingili (diski) zake, na kusababisha uchovu au maumivu ya muda mrefu. Hii ni kawaida kwa watu wanaofanya kazi za ofisini au kutumia muda mwingi mbele ya kompyuta bila mapumziko.

  1. Kubebesha mgongo mzigo kupita kiasi 
    Unapoinua vitu vizito hasa bila kutumia magoti na mkao sahihi, mishipa na misuli ya mgongo huweza kuchanika au kuvutika. Hili huenda likatokea mara moja (mfano, kwa kunyanyua kitu kizito ghafla) au taratibu kutokana na kujirudia kwa harakati hizo kwa muda mrefu inaweza kupelekea maumivu ya mgongo.

  1. Majeraha ya misuli au mishipa: Majeraha haya yanaweza kutokea wakati wa shughuli za kawaida kama kuinua vitu, au ajali kama kuanguka au ajali ya gari na vyombo vingine vya usafiri na hivyo kupelekea misuli kuvutika na kuumizwa ambapo inaweza kuvimba au kuwa na michubuko ya ndani, na matokeo yake ni maumivu makali au ya kudumu ya mgongo wa chini.

  1. Magonjwa ya uti wa mgongo 
  • Kupasuka au kuvimba kwa diski: hutokea diski inapobeba uzito mkubwa kupita kiasi hadi safu ya nje inapasuka na sehemu ya ndani kushinikiza neva. Hali hii husababisha maumivu makali ya mgongo au miguu.

  • Homa yabisi (Arthritis): Kwa mfano osteoarthritis husababisha uchakavu wa gegedu kati ya viungo vya uti wa mgongo na kutengeneza vinundu vya mfupa.  Uchakavu huu hutokana na matumizi ya mwili kwa muda mrefu. Diski zinapodhoofika, nafasi kati ya pingili hupungua hivyo kuongeza shinikizo na kusababisha maumivu na kufa ganzi.

  • Kubana kwa njia ya uti wa mgongo: Ni hali ambapo nafasi ya uti wa mgongo inapungua na hivyo kubana au kukandamiza mishipa ya fahamu (neva). Hali hii inaweza kuambatana na kuteleza kwa pingili za uti wa mgongo au magonjwa kama ugonjwa wa mifupa wa Paget.

  • Spondylolisthesis: Hutokea pale pingili moja inapoteleza mbele ya nyingine – mara nyingi kwa vijana, hasa wanamichezo, kutokana na jeraha. Kwa wazee, hutokana na uchakavu wa pingili. 

  1. Uzito kupita kiasi 
    Mzigo wa ziada unaosababishwa na uzito mkubwa wa mwili huongeza shinikizo kwa mgongo wa chini. Hii huathiri usawaziko wa mwili na kuongeza hatari ya kupata maumivu, hasa kwa watu wasiofanya mazoezi ya kutosha kuimarisha misuli ya mgongo. 

  1. Msongo wa mawazo: Husababisha misuli, hususani ya mgongo, kukaza kwa muda mrefu bila kulegea, jambo linalozuia mzunguko mzuri wa damu na kusababisha uchovu, kukakamaa, na maumivu sugu ya mgongo. 

Hali hii ikidumu huathiri pia usingizi, hamasa ya kufanya mazoezi, na hata kuongeza hisia za maumivu kupitia mabadiliko ya kihisia na kiakili, na kwa hivyo msongo wa mawazo unakuwa chanzo cha moja kwa moja na kisichoonekana cha maumivu ya mwili, hasa sehemu ya mgongo wa chini.

  1. Umri 
    Kadiri tunavyozeeka, mifupa na viungio hupoteza nguvu na ufanisi. Pingili kati ya uti wa mgongo hupoteza urefu na unyevunyevu wake, na kusababisha mgongo kupungua uwezo wake wa kunyonya mshtuko na hivyo kupelekea maumivu. 

Dalili za Maumivu ya Mgongo wa Chini ni Zipi? 

Maumivu ya mgongo wa chini yana dalili zifuatazo: 

  • Maumivu makali au ya kawaida  katika sehemu ya chini ya mgongo, ambayo yanaweza kuwa ya kudumu au yanayokuja na kuondoka. 

  • Kukakamaa kwa misuli ya mgongo, hasa baada ya kuinama, kunyanyua vitu, au kukaa kwa muda mrefu. 

  • Maumivu yanayoenea hadi miguuni, hasa paja au mguu mmoja, hali inayojulikana kama sciatica ikiwa mshipa wa sciatic umeathiriwa. 

  • Kuwashwa, kufa ganzi, au hisia za kuchomachoma  kwenye mgongo, makalio na hadi miguuni. 

  • Kupungua kwa uwezo wa kusogea au kunyumbulika, mtu huweza kuhisi mgongo kuwa mgumu au kushindwa kuinama.

  • Maumivu yanayoongezeka wakati wa kukaa, kusimama kwa muda mrefu, au kuinama, lakini hupungua unapolala au kupumzika. 

Maumivu ya Mgongo wa Chini Yana Tiba?

Yapo matibabu mabalimbali ya maumivu ya mgongo na mara nyingi tiba ya mgongo inahusisha wataalamu mbalimbali ambao wote ni muhimu katika kuleta matokeo mazuri kwa mgonjwa.

Lakini tafiti zinaeleza kwamba wagonjwa wa maumivu ya mgongo huwa wananufaika zaidi na tiba ya viungo (physiotherapy) hivyo katika makala hii nitaeleza ni kwa namna gani tiba hii inaweza kumsaidia mgonjwa mwenye maumivu ya mgongo.

Zifuatazo ni tiba za fiziotherapia kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maumivu ya mgongo wa chini: 

  • Mfiziotherapia hutoa elimu kwa mgonjwa juu ya tatizo, chanzo cha tatizo lake na namna tiba itakavyosaidia

  • Mazoezi tiba, ambapo mtaalamu wa fiziotherapia hutoa mazoezi yanayolenga kuimarisha misuli ya tumbo na mgongo na pia kuongeza unyumbulifi wa misuli kwa lengo la kupunguza ukakamavu na hivyo kutoa kabisa maumivu ya mgongo wa chini. 

  • Elimu juu ya mikao sahihi wakati wa kufanya kazi za ofisini husaidia kuweka msawazo katika misuli ya mgongo na pia kupunguza hatari ya kuongeza tatizo.  Pia mfiziotherapia hutoa kiti sahihi kinachosaidia kumweka mgonjwa katika mkao sahihi ambacho ni Ergonomic chair; husaidia mkao sahihi kazini au nyumbani kwa mgonjwa wa mgongo. 

  • Tiba ya joto na baridi ambayo inahusisha matumizi ya vifaa kama vile tiba ya joto kupunguza mkazo wa misuli (kwa kutumia heating pads), na barafu (cold packs) kupunguza maumivu ya mgongo wa chini. 

  • Tiba kwa kifaa cha umeme (electrotherapy) ambapo mfiziotherapia hutumia kichocheo cha umeme kama vile Transcutaneous electrical nerve stimulation (TENS) – kifaa ambacho huwekwa katika eneo la mgongo lenye maumivu na husaidia kupunguza maumivu ya mgongo wa shingo. 

  • Mvutano (lumbar traction machine), unaosimamiwa na Mtaalam wa tiba ya viungo.  Kifaa hiki hutumia uzani na puli, kuvuta mgongo wa chini polepole ili kupunguza mgandamizo wa mishipa ya fahamu na hivyo kutoa ahueni ya maumivu ya shingo – haswa kwa maumivu yatokanayo na kubanwa au kushinikizwa kwa mishipa ya fahamu inayotokea katika mgongo wa chini. 

  • Matumizi ya kifaa tiba maalumu cha kuvaa mgongoni kama vile Lumbo Sacral Belt na Lumbar Corset ambacho huimarisha mgongo na kupunguza shinikizo katika mgongo. 

Mwisho

Kwa kuwa maumivu ya mgongo yanaepukika kwa kiasi kikubwa ni vyema sasa kwa jamii kutambua umuhimu wa kujikinga dhidi ya maumivu ya mgongo wa chini kwa kuzingatia yale yote yaliyoelezwa katika makala hii.

Pia kuna haja ya kuhusishwa kwa wataalamu wengine wa afya pale inapohitajika. Bila kusahau kuchukua tahadhari mapema ya kumwona mtaalamu wa afya pindi uonapo dalili za maumivu ya mgongo wa chini ili kupata matibabu sahihi kwa wakati.

Kwa mahitaji ya huduma ya vifaa tiba vya physiotherapy na rehabilitation, usisite kuwasiliana nasi kupitia simu namba +255 767 226 702. Unaweza pia kutembelea akaunti yetu ya Instagram kwa maelezo zaidi kuhusu huduma zetu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *