Chanzo, Tiba na Namna ya Kujikinga na Maumivu ya Bega 

Je, unapata shida au maumivu wakati wa kuvaa koti au shati? 

Wewe ni mwalimu ukisimama darasani kuandika ubaoni na ghafla ukahisi bega lako limekaza kana kwamba linakataa kushirikiana?

Au baada ya kushiriki mchezo wowote (kama mpira wa kikapu), ukiamka asubuhi unahisi maumivu makali begani yanayokufanya kushindwa hata kuinua mkono?

Maumivu ya bega si jambo dogo la kupuuzia. Ni tatizo linaloathiri mamilioni ya watu duniani na ni la pili kwa ukubwa baada ya maumivu ya mgongo katika matatizo ya misuli na viungo. 

Tafiti zinaonyesha kuwa mtu 1 kati ya 4 atakutana na maumivu ya bega katika kipindi fulani cha maisha yake. Hali hii huathiri zaidi wale wanaofanya kazi zinazohitaji kutumia bega mara kwa mara: walimu, wachoraji, mafundi, wanamichezo, na wafanyakazi wa ofisini.

Kwa kuwa bega ni kiungo kinachohusika na harakati nyingi za kila siku (kuandika, kuinua, kubeba, au hata kugeuza mkono) ni rahisi kuumia, kuchoka kupita kiasi, au kuathirika na magonjwa ya uharibifu wa tishu. 

Ndiyo maana kuelewa chanzo cha maumivu ya bega ni hatua ya kwanza muhimu kuelekea tiba sahihi na kinga ya kudumu.

Katika makala hii, nitaeleza kwa undani, sababu zinazopelekea maumivu ya bega, njia za matibabu na tiba zinazopatikana, mbinu bora za kujikinga na maumivu haya ili kuendelea na maisha yenye afya na ufanisi.

Aina za Maumivu ya Bega

Maumivu ya bega yanaweza kuwa ya ghafla (acute) au ya muda mrefu (chronic). Acute hutokea ghafla, mara nyingi, kutokana na jeraha na hudumu kwa siku au wiki. Ya muda mrefu hutokea taratibu na hudumu kwa miezi au hata miaka.

Maumivu yanaweza kuwa sehemu moja ya bega au kusambaa hadi shingoni au mkononi.

Maumivu ya Bega Yanasababishwa na Nini?

Maumivu ya bega ni matokeo ya hitilafu katika tishu zinazounda bega ambapo hutokea kutokana na sababu mbalimbali kama magonjwa ya maungio (homa yabisi) na majeraha ya bega. 

Katika baadhi ya matukio, maumivu ya bega yanaweza kusababishwa na magonjwa ya ndani kama vile homa yabisi (arthritis) au hata mshtuko wa moyo. Kwa hiyo ni muhimu kuelewa sababu na matibabu yaliyopo ili kuyadhibiti ipasavyo. 

Zifuatazo ni sababu za maumivu ya bega:

1. Majeraha ya misuli inayoshikilia bega

Hii hutokea pale misuli (rotator cuff) na kano zinazoshikilia bega zinapoumia au kuharibika kutokana na kunyanyua vitu vizito, kazi za kurudia-rudia juu ya kichwa (kama kuandika ubaoni, ujenzi na michezo kama mpira wa kikapu), pia kuzeeka na uchakavu wa ungio la bega husababisha maumiu ya bega.

2. Kuvimba kwa kano (Tendons/impingement)

Hutokea pale kano zinapobanwa na mifupa wakati wa kuinua mkono juu. Hutokea zaidi  kwa watu wenye mkao mbaya au wanaofanya kazi za juu ya kichwa.

3. Kuvimba kwa kano au mfuko wenye maji (Tendonitis & bursitis)

4. Bega kuganda (frozen shoulder)

Hali ya bega kuwa gumu, kukaza na kupoteza uwezo wa kufanya harakati. Hutokea zaidi kwa watu wenye kisukari au waliokaa muda mrefu bila kutumia bega baada ya jeraha na hivyo kusababisha maumivu ya bega hasa wakati wa kutaka kulitumia bega.

5. Homa yabisi (arthritis)

Magonjwa ya maungio kama homa yabisi huchakaza bega na kusababisha maumivu, kukakamaa na mlio wa kukwaruza kwenye ungio la bega.

6. Kukandamizwa kwa mishipa ya  fahamu (nerve compression)

Hii hutokea pale neva inapobanwa shingoni au begani, ikisababisha maumivu yanayosambaa hadi mkononi, kufa ganzi, au ganzi.

7. Kuvunjika au kuteguka  kwa bega

Mfupa ukivunjika au bega likiteguka linaweza kusababisha maumivu makali, uvimbe, na hata mabadiliko ya umbo la bega.

Matibabu ya Maumivu ya Bega ni Yapi?

Yapo matibabu mbalimbali yanayoweza kutibu maumivu ya bega ikiwemo matumizi ya dawa za kupunguza uvimbe na maumivu kwa kufata ushauri wa wataalumu husika, tiba za viungo na hata upasuaji inategemea na kiasi cha jeraha na sababu zilizopelekea maumivvu hayo. 

Hivyo katika makala hii nitajikita katika tiba ya viungo yaani fiziotherapia ambapo nitaelezea ni kwa namna gani inaweza kumsaidia mgonjwa anayesumbuliwa na maumivu ya bega.

1. Kupumzika na kubadili shughuli

Ni vyema kupumzisha bega lako pindi unaposikia maumivu, kwa kufanya hivyo utakuwa umezuia kuongezeaka kwa jeraha katika bega. Nikiimanisha kwamba ikiwa ulikuwa unafanya shughuli za kubeba mizigo au kuinua mikono juu ya kichwa unapaswa kuacha ili upumzishe bega lako.

2. Barafu (cold pack) na joto (heating pads)

Kwa maumivu ya muda mfupi unapaswa kutumia barafu mara baada ya kuumia au kuanza kusikia maumivu na barafu inapaswa kutumika katika bega lenye maumivu kwa dakika 10 – 15 kupunguza uvimbe na maumivu.

Lakini kama maumivu yanasababishwa na kukamaa au kukaza kwa misuli ya bega utatumia tiba ya joto (heating pads) ili kulainisha misuli kwaajili ya kuondoa maumivu.

3. Mazoezi tiba

Mazoezi pia ni sehemu muhimu ya matibabu mfano mazoezi ya kuongeza uwezo wa kusogeza bega, mazoezi ya kuimarisha bega pamoja na mazoezi ya kuimarisha mbavu za bega. 

Haya yote yanapaswa kufanywa chini ya usimamizi wa mtaalamu wa tiba ya viungo (physiotherapist)

insta4. Matumizi ya vifaa tiba vya umeme kama TENS na Therapeutic ultrasound pia husaidia kupunguza au kuondoa maumivu ya bega.

“Ninajikinga vipi na maumivu ya bega?”

  • Kudumisha mkao sahihi na kuepuka kupinda shingo muda mrefu.
  • Kuimarisha misuli ya bega na mgongo wa juu kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara kwani hupunguza uwezekano wa kuumia kwa bega.
  • Epuka kuinua vitu vizito ghafla kwa kuongeza uzito polepole na tumia mbinu sahihi za kunyanyua mizigo.
  • Kupanga mazingira ya kazi vizuri kwa kutumia kiti chenye sapoti nzuri ya mgongo bila kusahau kuweka kompyuta au meza katika kiwango kinachokufaa.
  • Kupasha kabla ya kazi au michezo: Hii husaidia kupunguza mvutano wa misuli na kukuweka mbali na hatari ya kupata majeraha yanayoweza kupelekea maumivu ya bega.

Kumbuka: Usinyanyue mizigo mizito ghafla bila maandalizi, pia maumivu yanayoendelea zaidi ya wiki mbili yanahitaji ushauri wa daktari.

Mwisho

Maumivu ya bega ni tatizo linaloweza kuathiri maisha ya kila siku na kupunguza uwezo wa kufanya kazi au kushiriki katika shughuli za kawaida. 

Kwa kuwa bega ni kiungo kinachohusika na shughuli nyingi, ni rahisi kuumia au kuchoka kupita kiasi. Ndiyo maana ni muhimu kuelewa chanzo cha maumivu na kuchukua hatua sahihi za matibabu na kinga.

Hivyo, kila mtu ana wajibu wa kulinda afya ya mabega yake. Usipuuzie dalili ndogo kwani zinaweza kugeuka kuwa tatizo kubwa. 

Kwa ushauri zaidi wa kitaalamu, wasiliana nasi kupitia simu namba: +255 767 226 702

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *